UTANGULIZI
Kaliua ni miongoni mwa Halmashauri nane za Mkoa wa Tabora. Kijiografia, Kaliua ni njiapanda ya kwenda Kigoma na Katavi kwa kutumia njia ya Reli na Barabara. Pia Kaliua inaunganisha mkoa wa Kigoma na Shinyanga kupitia Uvinza na Kahama. Bustani, misitu na mabonde madogomadogo ndio mandhari inayokukaribisha unapoingia katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua mkoani Tabora. Unapovinjari ndani ya Halmashauri hii, kwa njiaya barabara, baadhi ya vitu utakavyoendelea kuona mbali na misitu, ni bustani za vitalu vya tumbaku na mabonde ya mpunga. Hadi sasa takribani 80% ya wakazi wa Kaliua wanajikita katika shughuli za kilimo na ufugaji wa mifugo mbalimbali pamoja na nyuki.
Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua ina eneo lenye ukubwa wa kilometa za mraba 14,050 ambalo ni sawa na asilimia 18.8 ya eneo la Mkoa wa Tabora. Eneo la Wilaya ya Kaliua linalotumika kwa makazi na kilimo/ufugaji ni asilimia 11 tu yaani kilometa za mraba 1,545.50 na eneo lililobaki 89% yaani kilometa za mraba 12,504.50 ni misitu ya hifadhi, mapori tengefu, mbuga na Maji. Makao Makuu ya Wilaya yapo katika Kata ya Kaliua, umbaliwa km 125 kutoka Tabora Mjini.
Kwa mwaka 2017 Wilaya ya Kaliua inakadiriwa kuwa na jumla ya watu 497,272. Kati ya hao wanaume ni 248,244 na wanawake ni 249,098. Ongezeko la idadi ya watu ni 4.8% na kaya zilizopo ni 75,460.
FURSA ZA UWEKEZAJI
Kutokana na ukweli kwamba, Wilaya ya Kaliua ipo kwenye mwinuko wa meta 1100m kutoka usawa wa bahari na joto ni la wastani wa 21.30C –33.00C, na hupokea kiasi cha mvua kati ya mm 900 – 1200 kwa mwaka, ardhi yenye rutuba, uoto wa asili uliorindimwa na miti aina ya miombo, mninga, mkurungu na mtundu.
Hata hivyo, kuwapo kwa mtandao wa barabara 843 km, reli, kiwanja cha ndege, huduma za kibenki na taasisi za huduma za kifedha, maji na umeme unaowezesha kuendesha mitambo inaifanya wilaya hii kuwa ni kivutio kwa uwakezaji katika sekta za mifugo, asali, kilimo, viwanda, utalii, elimu, afya na biashara.
RANCHI ZA MIFUGO
Wilaya ya Kaliua ina idadi kubwa ya mifugo ya aina mbalimbali ambapong’ombe ni 552,536, mbuzi 91,777, kondoo 17,441, nguruwe 5,250, sungura 196, punda 764, kuku 304,918, bata 17,968 na kanga 2,8
Pia kunasoko la uhakika la ndani na nje ya Wilaya la mifugo ambapo kwa mwaka 2016/17 - 2017/18 ng’ombe wapatao 33,190 na mbuzi 876 waliuzwa katika minada na kuwapatia wafugaji kipato cha shilingi bilioni 31.3.
ASALI
Wilaya ya Kaliua huzalisha tani 550 za asali kwa mwaka. Wazalishaji wakubwa ni vikundi 33 vya wafugaji nyuki na wafugaji binafsi. Ufugaji wa nyuki unafanyika katika misitu ya Mpandaline Forest Reserve, North Ugala, Luganzo Control area, Hifadhi ya Msitu wa Ulyankulu, Hifadhi ya Jumuiya ya ISAWIMA, na mapori ya vijiji na watu binafsi. Kulingana na uwepo wa misitu, mito, na vyanzo vingi vya maua na chakula cha nyuki, Wilaya ina uwezo wa kuzalisha zaidi ya tani 5,000 kwa mwaka. Hivyo, ufugaji wa nyuki katika Wilaya ya Kaliua, unatoa fursa za ufugaji wa nyuki, uanzishwaji wa viwanda vya kuchakata asali na mazao yatokanazo na asali kama vile nta, gundi, mvinyo, polishi na mishumaa.
TUMBAKU
Kaliua ni Mkoa wa Tumbaku kwani huzalisha zaidiya aslilimia 50 ya tumbuku yote Tanzania. Tunakaribisha wawekezaji na wakulima katika zao hili. Kulingana na wingi na uwezo mkubwa wa uzalishaji, tunakaribisha wawekezaji wakulima wakubwa na wadogo kuwekeza katika zao hili.
KOROSHO
Ardhi na tabia ya nchi ya Kaliua imethibitishwa kufaa kwa kilimo cha zao la Korosho. Hili ni moja ya zao la mkakati katika Wilaya ya Kaliua kutokana na maendeleo mazuri ya miche iliyokwisha pandwa na kutoa fursa ya uanzishaji wa viwanda Kwa kipindi 2020 mavuno ya korosho yanatarajiwa kuwa tani 672,000. Hivyo, tunakaribisha uwekezaji katika viwanda na kilimo cha korosho
KILIMO CHA UMWAGILIAJI
Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua ina mabonde makubwa yanayofaa kwa kuwekeza kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji yenye jumla ya hekta 9,200. Mazao kama Mpunga, Mhindi, Miwa, mbogamboga na matunda yanaweza kulimwa.
UFUGAJI WA SAMAKI
Kuna mito ya kudumu ya Ugala na Igombe na hivyo kuchochea ufugajI wa samaki kwa njia ya mabawa au vizimba. Maeneo yanayofaa kwa kazi yametengwa katika kata za Igagala, Zugimlole, Ushokola, Ilege na Usinge. Kwa sasa ufugaji unaofanyika ni wa asili na katika kipindi cha mwaka 2017/2018 wavuvi walivua samaki wapatao 200,789.
BIASHARA
Kaliua ina fursa nyingi za kiuwekezaji na biashara kama vile kuwekeza kwenye visima vya mafuta katika maneno ya Ulyankulu, Kaliua, Igagala na Usinge. Aidha tunakaribisha wawekezaji katika biashara usafiri na usafirishaji; huduma za shule, nyumba za kulala wageni, burudani na michezo
MADUKA YA DAWA
Wilayani Kaliua hadi sasa haina duka kubwa la madawa, maduka ya madawa yaliyopo yanatoa dawa muhimu na hayakidhi vigezo vya kusajiliwa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wateja wa bima ya afya (NHIF).
Hali hii inasababisha wanachama wa NHIF walio wengi kuwa na wakati mgumu wa kupata dawa pindi wanapozikosa katika vituo vya kutolea huduma za afya. Hivyo kwa sasa wateja wa NHIF wanalazimika kwenda Wilaya jirani kupata huduma hiyo.
UTALII
Kutokana na sababu mbalimbali za kihistoria, kiutamaduni na kijeografia zinaiweka Wilaya ya Kaliua katika fursa ya uwepo wa shughuli za utalii ambazo hutegemea vivutio vilivyopo na majira ya mwaka.
Vivutio hivyo ni kama vifuatavyo; Luganzo Game Controlled Area, kaburi la mtemi Milambo, maajabu ya milima ya Igwisi na njia ya utumwa Iselamagazi- Ulyankulu.
UWEZESHAJI NA MAWASILIANO
Halmashauri imeunda timu ya kuratibu shughuli zote za wawekezaji na uwekezaji. Tafadhali, kwa maswali, maoni, ushauri, au huduma za kujua fursa zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua tufikie kupitia:
Email: ded@kaliuadc.go.tz
Website: www.kaliuadc.go.tz
Simu:+255 622 225 618
+255 732 988 451
Mratibu: +255 627 022 034
Secretariat: +255 712 222 599
Ofisi zipo Eneo la Ufukutwa, Barabara ya Ulindwanoni
Sanduku La Posta: S. L. P 83 Kaliua
Simu: +255262965676/9
Dawati la Uwekezaji:
Barua Pepe: ded@kaliuadc.go.tz
Hatimiliki ©2016 Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua