Kiongozi wa mbio za mwenge 2018 Ndugu Charles Francis Kabeho, amezishauri Halmashauri nchini kuiga mfano kwa Halmashauri ya Kaliua. Akihitimisha zoezi la uwekaji mawe ya msingi na uzinduzi wa miradi Kabeho amesema kuwa ameridhishwa na usimamizi wa miradi na matumizi fedha za miradi yote aliyoitembelea kwani inaakisi thamani ya fedha (value for money) iliyotolewa na serikali pamoja na wahisani.
“Nampongeza sana Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkuu wa Wilaya, Mkurugenzi Mtendaji na wote walioshiriki katika usimamizi wa miradi hapa Kaliua” Alisema.
Mwenge wa uhuru ulipokelewa tarehe 24 Aprili katika eneo la Isawima ukitokea mkoani kigoma na kukimbizwa na wananchi katika vijiji vya Kaliua Magharibi, Imalampaka na Kaliua Mashariki.
Mbio za mwenge zimeweka mawe ya msingi na kuzindua jumla ya miradi nane yenye thamani ya shilingi 1,870,467,033.33 kutoka serikali kuu, Halmashauri, michango ya wananchi na wahisani.
Miradi iliyozinduliwa ni Jengo la ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua na Kiwanda cha mashine za kubangua karanga cha mtu binafsi Ndugu Fanuel Shao.
Wakati miradi iliyowekewa mawe ya msingi ni; Jengo la Upasuaji katika Kituo cha Afya Kaliua, Bweni la kulala wavulana shule ya sekondari Kaliua na Upanuzi wa ujenzi wa maghala ya kuhifadhia nafaka kwa Ndugu Jumanne Lusaba.
Miradi mingine iliyowekewa mawe ya msingi ni ujenzi wa stendi ya mabasi, egesho la malori na kibanda cha abiria pamoja na Mradi wa ujenzi wa barabara kilometa moja kwa kiwango cha lami. Vile vile mwenge wa uhuru ulikagua mabanda ya upimaji wa UKIMWI/VVU, Banda la wapinga rushwa, wapinga matumizi madawa ya kulevya, banda la wajasiriamali vijana na wanawake na kutoa zawadi za washindi wa mpira wa miguu wa ligi ya mwenge. Sambamba na uzinduzi wa miradi wakimbiza mwenge walipata fursa ya kupanda miti katika maeneo mbalimbali.
Wananchi wa Kaliua walishiriki katika mkesha wa sherehe za mwenge uliofanyika katika viwanja vya Kolimba na kuwapa fursa ya kupima virusi vya ukimwi malaria na kuchangia damu.
Mkuu wa Wilaya ya Kaliua Mh. Abel Yeji Busalama amehitimisha mbio za mwenge wilayani kaliua na kuukabidhi mwenge kwa Mkuu wa wilaya ya Urambo Bi. Angelina Kwingwa 25.04.2018 ukiwa unawaka na kumeremeta.
Ofisi zipo Eneo la Ufukutwa, Barabara ya Ulindwanoni
Sanduku La Posta: S. L. P 83 Kaliua
Simu: +255262965676/9
Dawati la Uwekezaji:
Barua Pepe: ded@kaliuadc.go.tz
Hatimiliki ©2016 Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua